Waziri mpya wa fedha Afrika Kusini awekewa shaka, ajieleza

0

WAKATI Chama tawala cha Afrika Kusini  (ANC) kimegawanyika baada ya Rais Jacob Zuma kumtema Waziri wa Fedha Pravin Gordhan, mteule mpya, Malusi Gigaba, ambaye ameapishwa jana amesema kwamba atahakikisha anatekeleza sera za chama hicho.

Wataalamu wanasema kwamba uteuzi wa Gigaba umeonesha mgawanyiko mkubwa uliopo ndani ya chama cha ANC.

Kuondolewa kwa Pravin Gordhan, Alhamisi iliyopita kumeleta mtikisiko mkubwa.

Akizungumza na waandishi wa habari  alisema kwamba kazi yake kubwa ni kuhakikisha kwamba  sera za ANC  zinatekelezwa ili kuwaletea nafuu wananchi wa Afrika Kusini.

Mwaka 2014,  ANC ilipitisha sera ambazo zilitaka mabadiliko ya haraka ili kuwawezesha waafrika kuingia katika umiliki na uendeshaji wa uchumi wa taifa hilo.

Gigaba amesema kwamba kumekuwepo na makubaliano ndani ya ANC kwamba mabadiliko yaliyokusudiwa yanaenda polepole na tena mahali pengine mabadiliko hayo hayana manufaa sana kwa wananchi.

Uteuzi wa Gigaba, ambaye alikuwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani, umeleta kiwingu kwa upinzani na wachumi ambao wanamuona kwamba hafai na ni rafiki wa Zuma.

Gigaba amesema pamoja na kujua namna, fitina za kisiasa, zilivyo kwa sasa nchini Afrika Kusini, yeye atawajibika katika kazi zake na wala hatasikiliza wimbi hilo la fitina.

Alisema anaelewa shaka za watu kuhusu uteuzi wake lakini atafanya vyema katika kazi zake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here