Jengo la bunge lachomwa kupinga mabadiliko ya katiba

0

WAANDAMANAJI nchini Paraguay wamechoma moto jengo la Bunge la nchi hiyo wakipinga muswada wa kuondoa muda wa utawala kwa Rais wa taifa hilo.

Polisi walilazimika kutumia risasi baridi kutawanya  wanadmanaji hao na katika purukushani hizo mtu mmoja alipoteza maisha.

Chini ya katiba ya mwaka 1992 baada ya kuondolewa kwa utawala wa kidikteta, Rais wa nchi hiyo alikuwa anahudumu kwa kipindi kimoja cha miaka mitano.

Imeelezwa kuwa Rais wa sasa, Horacio Cartes anataka kutumikia kipindi cha pili na hivyo anafanya mipango ya kubadilishwa kwa katiba.

Waandishi wa habari walishuhudia waandamanaji wakivunja vioo na kuanzisha moto ndani ya jengo hilo.

Imeelezwa kuwa waandamanaji hao walivamia pia ofisi  za wanaounga mkono muswada huo wa kubadilisha muda wa utawala.

Polisi pamoja na kutumia risasi za baridi walilazimika  pia kutumia maji ili kutawanya waandamanaji.

Rais Horacio Cartes.

 

Shirika la habari la Ufaransa (AFP) limesema kwamba takaribani watu 30 wamejeruhiwa wakiwamo wabunge watatu na seneta mmoja.

Imeelezwa kuwa jengo la Bunge liliwaka moto kwa saa mbili kabla kikosi cha zimamoto kufanikiwa kuudhibiti.

Aidha vurugu hizo za kwanza za aina yake tangu taifa hilo kuingia katika utawala wa kidemokrasia mwaka 1992, zinaelezwa kuleta kovu kubwa katika demokrasia ya nchi hiyo.

Hata hivyo mwanaharakati wa upinzani Rodrigo Quintana, 25, aliuawa katika ghasia hizo wakati askari walipovamia ofisi ya chama cha upinzani cha Liberal . Taarifa ya kifo hicho ilitolewa na Kiongozi  wa chama hicho, Efrain Alegre.

Polisi wanasema kwamba wameanzisha uchunguzi kujua chanzo halisi cha kifo cha mwanaharakati huyo.

Muda wa uongozi wa Cartes unatarajia kumalizika mwakani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here